Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, katika hali ya kuongezeka kwa changamoto zinazoikabili dunia ya Kiarabu na Kiislamu, pamoja na kukua kwa miradi ya Marekani na Israel inayolenga kuipanga upya kanda kwa misingi ya kisiasa, kiusalama na kiuchumi inayotumikia maslahi ya wavamizi, “Umoja wa Kiislamu” unaonekana kuwa chaguo linalovuka mipaka ya tukio la msimu au la muda, na kuwa ulazima wa kimkakati wa kulinda utambulisho wa Umma na kuimarisha uwezo wake wa kukabiliana na miradi ya kuleta mgawanyiko.
Katika muktadha huo, Sheikh Mu’min Al-Rifa‘i, mwanazuoni wa Kisunni na mshauri wa masuala ya uhusiano wa kidiplomasia nchini Lebanon, katika mazungumzo na tovuti ya habari ya «Al-Ahed», alisisitiza: “Wiki ya Umoja wa Kiislamu,” ambayo inaambatana na kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Mtukufu (s.a.w.w.), ni tukio linalowaunganisha watu wote wa Umma, na umoja si kaulimbiu ya muda mfupi inayopita, bali ni uzoefu ambao ulazima wake umethibitika katika kukabiliana na mashambulizi na miradi ya kikoloni.
Alimtumia salamu Imam Khomeini na Imam Sayyid Ali Khamenei (q.s.), na kupitia upya nafasi yao katika kuimarisha dhana ya Umoja wa Kiislamu na kuzibadilisha tofauti kuhusu tarehe ya kuzaliwa Mtume kuwa tukio linalozalisha umoja.
Alifafanua kwamba; kuweka kipindi cha kuanzia tarehe 12 hadi 17 Rabiul-Awwal kuwa “Wiki ya Umoja wa Kiislamu” kulitoa fursa ya kuvuka tofauti kuhusu siku ya kuzaliwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (s.a.w.w.), na kuibadilisha tofauti hiyo kuwa uwanja wa kukutana na kuungana; kiasi kwamba kuzaliwa kwa Mtume, badala ya kuwa chanzo cha mgawanyiko, kukawa tukio la kuwakusanya pamoja watu wote wa Umma huu.
Anaamini kwamba Wiki ya Umoja wa Kiislamu imekuwa katika dhamira ya Umma kuwa tukio jumuishi linaloweza kuhuisha mambo makubwa yanayowakutanisha Waislamu, yakiongozwa na kumuamini Mtume Mtukufu Muhammad (s.a.w.w.) na ujumbe wa Uislamu, na kufungua njia ya kujenga umoja unaovuka tofauti za kimadhehebu na kihistoria.
Marekani na “Israel” zinatumia fursa ya mgawanyiko
Sheikh Al-Rifa‘i, akionya kwamba Marekani na utawala wa Israel katika sera zao kuelekea eneo hili hawatendi kwa nia ya kulinda maslahi ya madhehebu, kabila au jamii fulani, alisisitiza: “Mkakati wa Marekani na Israel umejengwa juu ya kutimiza maslahi ya kiuchumi, kisiasa, kijeshi na kikoloni katika eneo.”
Alisema: “Washington na Tel Aviv hawatafuti maslahi ya Ahlus-Sunna wal-Jamaa, wala maslahi ya Mashia Ithnaasharia au Mashia Zaidiyya, wala maslahi ya Waarabu; bali wanafanya kazi kwa misingi ya hesabu za kimkakati zinazohudumia mradi wa Israel na sera za Marekani katika eneo.”
Aliongeza: “Kukabiliana na miradi hii huanza kwa kuielewa asili yake, kwa sababu adui hutumia hali ya mgawanyiko na utengano katika jamii za Kiislamu, wakati umoja ni sababu ya nguvu inayozuia tofauti za kimadhehebu na kisiasa kugeuzwa kuwa nyenzo za kuisambaratisha jamii.”
Uzoefu wa Iran na Lebanon
Sheikh Al-Rifa‘i aliutaja uzoefu wa kiutendaji katika eneo hili kuwa ushahidi kwamba Umoja wa Kiislamu si dhana ya kinadharia, bali ni kipengele cha msingi katika kusimama imara na kukabiliana na changamoto. Alieleza kwamba Iran, kutokana na kuwepo kwa hali ya mshikamano na umoja wa ndani, iliweza kusimama dhidi ya mashambulizi ya Marekani na Israel.
Aidha, alizungumzia hali ya Lebanon na anaamini kwamba Muqawama nchini Lebanon umejengwa juu ya mazingira imara ya uungaji mkono wa wananchi, na kwamba mazingira hayo hayawezi kuwekwa katika mipaka finyu ya kimadhehebu, bali ni mazingira jumuishi yenye vipengele mbalimbali.
Alisema: “Nguvu ya Muqawama haitokani na uwezo wake wa kijeshi pekee, bali pia inatokana na wafuasi wake, wananchi na mazingira yake ya uungaji mkono.” Alisisitiza kwamba kukusanyika kwa watu wote wa Umma katika kukabiliana na mashambulizi, kwa asili yake, kunategemea Uislamu na Umoja wa Kiislamu.
Uzoefu wa moja kwa moja wa kijeshi na mapambano dhidi ya maadui wa Umma umethibitisha ufanisi na ulazima wa Umoja wa Kiislamu, hususan katika mazingira ya juhudi za mradi wa Kizayuni na Marekani za kupanua ushawishi wao katika eneo na kulazimisha hali mpya kwa watu wa eneo hilo.
Kuigeuza Wiki ya Umoja kuwa mradi wa kiutendaji
Kuhusiana na namna ya kutumia mazingira ya Wiki ya Umoja wa Kiislamu katika kukabiliana na ubeberu wa Marekani na Israel na kuimarisha utamaduni wa Muqawama, Sheikh Al-Rifa‘i alisisitiza umuhimu wa kutoridhika na kuihuisha kumbukumbu hiyo kwa namna ya sherehe pekee, bali akataka kuwepo kwa juhudi endelevu za kuhuisha tena dhana ya umoja na kuchochea uwepo wake katika nyanja za kiutamaduni, kijamii na kisiasa.
Anaamini kwamba kuimarisha umoja kunahitaji kuimarisha misingi yake ya kiutamaduni. Alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushiriki wa Waislamu wa madhehebu mbalimbali katika shughuli za wenzao; kwa namna ambayo wafuasi wa madhehebu ya Shia washiriki katika sherehe za ndugu zao wa Ahlus-Sunna, kama ambavyo Ahlus-Sunna washiriki katika hafla zinazofanywa na makundi ya Shia kwa ajili ya kuhuisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Mtukufu (s.a.w.w.) na Wiki ya Umoja wa Kiislamu.
Alisisitiza kwamba; hatua kama hizo zinaweza kuimarisha mahusiano na mawasiliano kati ya watu wote wa Umma na kutuma ujumbe ulio wazi kwamba Waislamu, licha ya tofauti zao za kimadhehebu, wanaweza kusimama bega kwa bega katika kukabiliana na changamoto kubwa zinazoilenga kanda yao.
Alisema: “Kinachohitajika ni kusisitiza kwamba Ahlus-Sunna na Shia bado wanaweza kukusanyika katika safu moja na chini ya mwamvuli mmoja wa Kiislamu; mwamvuli wa Uislamu, na kwa mfano mmoja; Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad (s.a.w.w.).”
Umoja huanza kwa kuuelewa ujumbe wa Kiislamu
Sheikh Al-Rifa‘i alisisitiza umuhimu wa kuongeza shughuli za kiutamaduni, kisiasa na kiakili zinazochunguza malengo ya ujumbe wa Uislamu na “Wiki ya Umoja wa Kiislamu,” akisema kwamba kurejea katika malengo hayo kunapelekea kufikiwa kwa uelewa wa kina zaidi kuhusu ujumbe aliokuja nao Mtume Muhammad (s.a.w.w.).
Kwa mtazamo wake, kuimarisha mshikamano na kujihusisha na Uislamu na Mtume Mtukufu Muhammad (s.a.w.w.) hakutimizwi kupitia kaulimbiu pekee, bali kupitia kujenga upya uelewa kuhusu ujumbe wa Kiislamu na malengo yake; kwa namna inayolinda utambulisho wa Umma na kuimarisha uwezo wake wa kushiriki na kuwa na ushawishi.
Alisema: “Umma wa Kiislamu unajumuisha karibu Waislamu bilioni mbili, lakini ukubwa wake wa idadi si lazima uakisi kiwango cha ushawishi na ufanisi wake. Kinachohitajika ni kuibadilisha idadi hii kubwa ya watu wa Kiislamu kuwa nguvu hai, yenye kuzalisha na yenye uwezo wa kuacha athari yake duniani.”
Alisema: “Kinachohitajika si Waislamu bilioni mbili kwa upande wa idadi pekee, bali Waislamu bilioni mbili wenye utambulisho ulio wazi, wenye uzalishaji, walio hai na walioshiriki, ambao wataruhusu Umma kuwa na uwepo wenye ushawishi katika ulimwengu.”
Msikiti; kitovu cha maisha, si mahali pa kujitenga
Sheikh Al-Rifa‘i aliendelea kuzungumzia nafasi ya msikiti katika kuijenga jamii, akisisitiza: “Uislamu haukuja kumtenga mwanadamu na maisha, bali umekuja na ujumbe wa maisha jumuishi.”
Alieleza kwamba; katika uzoefu wa mwanzo wa Kiislamu, msikiti haukuwa mahali pa ibada kwa maana finyu pekee, bali ulikuwa kituo cha kusimamia mambo ya jamii na mahali pa utawala, uongozi, elimu, masuala ya kijamii, ulinzi na uhusiano wa nje.
Alifafanua kwamba kuhuisha tena nafasi hii ya msikiti kunaweza kuwa njia ya msingi ya kulea vizazi kwa misingi ya Uislamu jumuishi, mbali na migawanyiko inayochosha na kudhoofisha jamii za Kiislamu.
Alisisitiza umuhimu wa kuufanya msikiti kuwa kituo kikuu cha malezi, uongozi na kukuza vizazi; msikiti unaojengwa juu ya msingi wa Uislamu safi wa Muhammad na Umoja wa Kiislamu, ili uwe mahali pa kuunganisha, na kuviunganisha tena vizazi na ujumbe wa Mtume Mtukufu (s.a.w.w.).
Kulea vizazi kwa misingi ya umoja kunaukinga Umma
Sheikh Al-Rifa‘i alihitimisha kauli zake kwa kusisitiza kwamba; kujenga Umoja wa Kiislamu huanza kwa kuvilea vizazi vipya juu ya msingi wa kuelewa kiini cha Uislamu na malengo ya ujumbe wake. Anaamini kwamba uelewa huu ni ngome muhimu zaidi dhidi ya miradi ya kuleta mgawanyiko inayolenga Umma.
Anaamini kwamba kuelewa malengo ambayo wazo la “Wiki ya Umoja wa Kiislamu” lilijengwa juu yake na kuyathibitisha katika uelewa wa kizazi kipya, kunatosha kuimarisha usalama wa jamii za Kiislamu dhidi ya miradi ya Marekani, Israel na miradi mingine inayolenga kuigawa kanda na kuipanga upya kwa namna inayotumikia maslahi yao.
Alisisitiza: “Wakati Umma unapoungana juu ya uelewa wa pamoja kuhusu ujumbe wa Uislamu na malengo yake, na unapozichukulia tofauti zake kuwa uwanja wa utofauti badala ya kuzifanya kuwa kisingizio cha mzozo, uwezo wa maadui kutumia mgawanyiko hupungua, na Umoja wa Kiislamu hugeuka kuwa nguvu halisi ya kulinda utambulisho, maslahi na mustakabali wa mataifa ya eneo.”
Maoni yako